Jumatatu 23 Novemba 2026 - 14:00
Ndoto ya mtoto wa Kipalestina/ Laiti ningeliweza kuwa na furaha

Hawza/ Mtoto wa miaka kumi kutoka Ghaza, anayeitwa Mujahid, amewapoteza wazazi wake katika vita vya utawala wa Kizayuni. Kwa sasa, meno yake na mkono wake vimevunjika kutokana na nguvu ya mlipuko, huku mguu wake ukiwa umejeruhiwa na kumfanya achechemee. Aidha, anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani, lakini hana huduma wala vifaa vya kumwezesha kupata matibabu.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, mahojiano haya yanamhusu Mujahid, mtoto wa miaka kumi kutoka Ghaza, yaliyofanywa na wanaharakati wanaojihusisha na shughuli za kibinadamu.

Baada ya wazazi wa Mujahid kufariki dunia, mjomba wake alichukua jukumu la kumlea. Hadi hivi karibuni, Mujahid alikuwa akiishi katika hema moja pamoja na mjomba wake, shangazi yake na binamu zake wawili yatima, ambao pia walikuwa chini ya uangalizi wa mjomba huyo.

Wazazi wote wawili wa Mujahid waliuawa wakati nyumba yao ilipobomolewa. Tukio hilo halikumfanya mtoto huyo kuwa yatima tu, bali pia lilimsababishia majeraha makubwa.

Mujahid anakabiliwa na majeraha makubwa yaliyosababisha kuvunjika meno na mkono wake. Hali hiyo imemfanya ashindwe kuzungumza na kula kama kawaida. Mbali na maumivu anayoyapata, hali hiyo pia humletea aibu.

Anasema: “Sina wazazi ambao wangeweza kugharamia matibabu ya meno yangu. Laiti ningeliweza kupata huduma za matibabu ninazohitaji, ili niweze kuzungumza, kula na kutabasamu kama watoto wengine.”

Mguu wa Mujahid pia umejeruhiwa, na sasa anatembea kwa kuchechemea. Pia hupata shida kutembea umbali mrefu.

Watu wazima nchini Ghaza wanafanya kila wawezalo kuwasaidia watoto. Mlezi wa Mujahid naye amejitahidi sana kama wengine, lakini hana uwezo wa kugharamia matibabu ya meno ya mtoto huyo.

Badala yake, familia hiyo imelazimika kuyapa kipaumbele matibabu ya kemotherapi kwa ajili ya saratani ya damu inayomsumbua Mujahid. Kwa mujibu wa chanzo cha habari hii, ugonjwa huo umetokana na kemikali zilizotumiwa na utawala wa Kizayuni. Matibabu hayo humlaza kitandani kwa siku kadhaa, huku akipitia hali ya maumivu na uchovu.

Mwanzoni mwa mwezi Novemba, hali ya familia hiyo ilizidi kuwa mbaya baada ya mafuriko makubwa kusababisha hema lao kuanguka na kuharibu baadhi ya mali zao. Hatimaye, familia hiyo ilihamia pamoja na ndugu zao katika jengo lililokuwa limeharibika kwa sehemu, lililopo karibu na eneo hilo.

Kuta za jengo hilo zimekuwa nyeusi kutokana na moto uliowahi kutokea hapo awali. Milango, madirisha na matundu yaliyopo ukutani vimefunikwa kwa turubai, ambazo hazina uwezo wa kuzuia upepo wa baridi wa majira ya baridi. Hata hivyo, kwao, kupata hifadhi ndogo ni afadhali kuliko kukosa makazi kabisa.

Licha ya changamoto zote hizo, Mujahid amejiunga na kituo cha elimu cha muda kilichopo katika kambi ya wakimbizi iliyo karibu. Ingawa mazingira ya kujifunzia si mazuri, mtoto huyo amedhamiria kuendelea na masomo yake. Aidha, anapata msaada wa mwalimu binafsi ili kufidia masomo yote aliyokosa kutokana na janga linaloendelea.

Chanzo: islamic-relief.org

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha